HISTORIA (WASIFU WA) YA MAREHEMU DKT. WILLIAM AUGUSTAO MGIMWA (MB) ALIYEKUWA WAZIRI WA FEDHA KATIKA SERIKALI YA AWAMU YA NNE YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 1. KUZALIWA Marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa alizaliwa tarehe 20 Januari, 1950 katika kijiji cha Magunga, mkoa wa Iringa. 2. ELIMU Marehemu Dkt. William Mgimwa alianza elimu ya msingi katika shule ya Msingi WASA mwaka 1961 hadi 1965. Alijiunga na shule ya kati (Middle School) ya Tosa kuanzia mwaka 1965 hadi mwaka 1967. Kwa upande wa elimu ya sekondari, marehemu Dkt. Mgimwa alisoma katika shule ya Seminari ya Tosamaganga mwaka 1968 mpaka 1969 na shule ya Seminari ya Mafinga mwaka 1970 hadi 1971. Mwaka 1975 hadi mwaka 1978, marehemu Dkt. Mgimwa alisomea na kupata stashahada (Advanced Diploma) ya masuala ya kibenki katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha -IFM. Mwaka 1983 hadi 1984 alipata Postgraduate Diploma, ya masuala ya fedha katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha. Mwaka 1989 hadi 1991, marehemu Dkt. Mgimwa alisoma na kupata Shahada ya Uzamili (MBA-Finance) ya masuala ya fedha katika Chuo cha Uongozi Mzumbe, wakati huo kikiitwa Institute of Development Management(IDM). 1
Mwaka 2003, marehemu Dkt. Mgimwa alitunukiwa Shahada ya juu ya Uzamivu ya Masuala ya Fedha yaani Doctor of Philosophy (Ph.D) in Finance Aidha, marehemu Dkt. Mgimwa amehudhuria mafunzo mbalimbali ya masuala ya fedha ndani na nje ya nchi pamoja na kupelekwa Attachment kumjengea uwezo katika Taasisi mbalimbali zikiwemo; Bank of England mwaka 2001, Chuo cha Benki ya ABSA, Afrika Kusini, 2000, Chuo cha Benki Kuu ya India,2003 IMF, Washington, 2001 Bank for International Settlement, Switzerland Kwa watumishi wengi nchini na hasa wale wa mabenki na vyombo mbalimbali vya fedha watamkumbuka marehemu Dkt. Mgimwa kama Mwalimu na Mlezi. Mbali na kufundisha, marehemu Dkt. Mgimwa ameandika na kuhariri vitabu kadhaa vikiwemo Advanced Credit Operations 2006/7 na Advanced Treasury Management 2008/9. Aidha, Marehemu Dkt. Mgimwa amechapisha makala kadhaa yanayohusu sekta ya uchumi na fedha katika majarida mbalimbali ndani na nje ya nchi. 3. AJIRA Kuanzia mwaka 1980 hadi 1981, marehemu aliajiriwa na kufanya kazi katika Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce-NBC) kama Mhasibu (Bank Accountant). Mwaka 1981 alihamishiwa Tawi la NBC Mtwara akiwa Meneja wa Tawi (Branch Manager) 2
Mwaka 1982 hadi 1989, alifanya kazi kama Mhadhiri (Instructor/Trainer) katika Chuo cha Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Iringa. Mwaka 1996 hadi 1997 alikuwa Meneja Mkuu (Chief Manager) wa Benki ya Taifa ya Biashara(NBC), akishughulikia Mafunzo na Bajeti. Mwaka 1997 hadi 2000, alipanda cheo na kuwa Mkurugenzi (Director of Corporate Services) katika benki hiyo hiyo ya NBC, akishughulikia masuala ya Usimamizi wa mikopo na operesheni za Kimataifa. Mwaka 2000 hadi 2010, aliajiriwa Benki Kuu ya Tanzania akiwa Mkurugenzi na Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kilichopo jijini Mwanza. Kuanzia Mei, 2012 alikuwa Waziri wa Fedha hadi mauti yalipomkuta. 4. MAISHA YA SIASA Kati ya mwaka 1991 hadi 1994, marehemu Dkt. W. Mgimwa alikuwa Diwani wa Kata ya Gangilonga, mkoani Iringa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. Mwaka 1994 hadi 1995 alikuwa Kamanda Msaidizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Iringa. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 alikuwa Mlezi wa Kata ya Wasa mkoani Iringa. Mwaka 2010 hadi 2014 mauti yalipomkuta, marehemu alikuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa. Aidha, baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, Marehemu Dkt. Mgimwa amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge iliyokuwa ya Fedha na Uchumi. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Dkt. William A. Mgimwa kuwa Waziri wa Fedha kuanzia mwezi Mei 2012. 3
Kwa wadhifa wake aliokuwa nao ulimfanya pia awe;pamoja na nyadhifa nyingine: Mjumbe wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Masuala ya Fedha na Uchumi, Gavana katika Benki ya Dunia, Gavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, Gavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB, Mjumbe wa Baraza la Uongozi (Governing Council) la Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), na Mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya PTA Bank. Kutokana na ujuzi na uzoefu wake, marehemu Dkt. Mgimwa amekuwa akitoa mchango mkubwa na kupewa nafasi za kuwa mwenyekiti na mzungumzaji mkuu kwenye mikutano ya kimataifa. 5. KUUGUA Marehemu Dkt. William Mgimwa alienda nchini Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 3 Novemba, 2013 kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake katika Hospitali ya Kloof Medi Clinic iliyoko Pretoria. Baada ya Uchunguzi Madaktari walishauri alazwe kwa uangalizi zaidi na matibabu. Akiwa amelazwa Hospitalini, aliendelea na matibabu hadi mauti ilipomfika kutokana na tatizo la figo. 6. KUFARIKI Marehemu Dkt. W. Ngimwa alifariki Mwaka Mpya, Jumatano tarehe 1 Januari 2014 saa 6.25 mchana saa za Afrika Mashariki katika Hospitali hiyo ya Kloof Medi- Clinic. 4
7. HITIMISHO Marehemu Dkt. William Mgimwa ameacha Mjane Bi. JANE KAKINGU na watoto saba (7) ambao ni MARIO, FLORA, GODFREY, FELIX, SCOLA, JAMES na DENNIS. BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA LIHIMIDIWE +++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++ 5